Jumanne , 2nd Dec , 2014

Utafiti uliofanywa na Mtandao wa Madeni na Maendeleo nchini Tanzania TCDD, umebaini mapungufu makubwa katika usimamizi wa madeni, ambapo zaidi ya wizara Tisa za serikali zinahusika katika ukopaji, uidhinishaji na usimamizi wa deni la taifa.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo nchini Tanzania - TCDD, Bw. Hebron Mwakagenda.

Mkurugenzi wa TCDD Bw. Hebron Mwakagenda amesema hayo wakati akitoa ripoti ya utafiti huo jijini Dar es Salaam leo, ripoti ambayo pamoja na mambo mengine, imeibua tuhuma za aina mpya ya ufisadi unaofanyika kupitia utaratibu wa dhamana ya mikopo inayotolewa na serikali kwa makampuni mbalimbali nchini.

Mwakagenda amesema utafiti umebaini kuwa licha ya sheria kumpa waziri wa fedha mamlaka ya kukopa kwa niaba ya serikali, bado watumishi kadhaa wa umma wamekuwa wakitoa maamuzi ya kukopa pasipo kuwa na idhini ya kisheria kufanya hivyo.

Aidha, Mwakagenda ameongeza kuwa Tanzania imefikia hatari ya kuwa nchi isiyokopesheka kutokana na kutokwepo kwa uwiano baina ya deni na pato la ndani ya taifa, hukua akionesha wasiwasi kuwa huenda hata deni lenyewe likawa kubwa kuliko inavyoelezwa hivi sasa na serikali.