Jumamosi , 21st Feb , 2015

Tanzania inaunga mkono kwa dhati Ushirikiano wa Kikanda na muumini mkubwa wa Umoja wa Afrika na Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akimkabidhi rasmi Rais Kikwete uenyekiti wa EAC

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema jijini Nairobi mara baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa EAC na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye amekuwa mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Rais  Kikwete ampongeza Rais Kenyatta kwa kusimamia utekelezwaji wa maazimio na miradi ya pamoja ya Jumuiya wakati wa kipindi chake cha uenyekiti na kuahidi kuwa Tanzania haitawaangusha wana Afrika Mashariki katika kutekeleza azma yao ya pamoja ya kuendeleza Jumuiya hiyo.

Rais Kikwete amesema katika utekelezaji wa ajenda ya EAC, biashara imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kwamba nchi zote wanachama zinayaona matunda hayo.

Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2013 biashara katika nchi za EAC imeongezeka kutoka dola za kimarekani 3, 722.9 hadi dola 5,805.6 ambapo kati ya mwaka 2012 hadi 2013 kumekuwa na ongezeko la asilimia 6.

Rais Kikwete amesema biashara isiyo rasmi ingerasimishwa, ongezeko la biashara lingekuwa juu zaidi, hivyo imefikia wakati muafaka wa kurasimisha biashara isiyo rasmi katika ushirikiano huo.

Rais Kikwete amerejea nyumbani mara baada ya mkutano huo ambao umehudhuriwa na Marais wa nchi zote tano za Jumuiya na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ambaye amehudhuria kama mualikwa maalum katika kipindi hiki ambapo mazungumzo ya awali ya kuijadili nchi yake kama inaweza kupata uanachama katika EAC yanaendelea.