Ijumaa , 15th Mar , 2024

Tanzania kupitia Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, imefanya mazungumzo na Waziri wa Miundombinu wa Burundi Mhe. Dieudonné Dukundane, kuhusu maendeleo ya Mradi wa Reli ya Kisasa SGR utakaoziunganisha nchi hizo mbili.

Ujumbe wa Tanzania (Kushoto) ukiongozwa na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (katikati kushoto), na Ujumbe wa Burundi ukiongozwa na Waziri wa Miundombinu na Makazi, Mhe. Dieudonne Dukundane (katikati kulia), wakiwa katika kikao cha pamoja, kilichofanyika jijini Dodoma, kilichojadili kuhusu Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) itakayounganisha nchi hizo mbili.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Dodoma, Viongozi hao wamesema kuwa mradi huo utakapokamilika utachochea biashara ya madini na kilimo pamoja na kuimarisha mahusiano ya kikanda na kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa Dkt. Nchemba, Ushirikiano wa nchi hizo mbili katika maandalizi ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) umekua mzuri na kwamba watalaamu wa pande zote mbili wameendelea na vikao hususan katika eneo la manunuzi na fedha ili kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa.

“Ujenzi wa Reli hii ya Kisasa ya kuunganisha nchi zetu ni muhimu sana kwetu na maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ni mradi wa Kipaumbele na anataka ukamilike” aliongeza Mhe Dkt. Nchemba

Alisema kuwa wataalum kutoka nchi hizo mbili wanaendelea kushirikiana ili kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa na kufikia matarajio ya Rais wa Tanzania pamoja na Rais wa Burundi ya kuona mradi huo unafanikiwa.

Naye Waziri wa Miundombinu na Makazi wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Dieudonné Dukundane, alisema kuwa nchi yake itahakikisha kuwa mradi huo unapewa kipaumbele na tayari timu ya wataalam kutoka Burundi ipo Dar es Salaam ikiendelea kupitia masuala ya manunuzi wakishirikiana na wataalam wa Tanzania.

“Rais wangu Mhe. Evariste Ndayishimiye, ametuelekeza kuwa tufuatilie kwa ukaribu na kwa kipaumbele mchakato mzima unakwenda kama ilivyopangwa ili uishe vizuri, na mimi nimeishi hapa Tanzania kwa miaka sita (6) nimeona namna ambavyo SGR itakavyoharakisha maendeleo ya nchi” alisema Mhe. Dukundane.

Mradi huo wa Reli ya Kisasa (SGR) baada ya kukamilika hususan Ujenzi wa Reli ya Uvinza hadi Musongati nchini Burundi kutawezesha kusafirisha tani milioni 3 za madini kwa mwaka kutoka mgodi mkubwa wa madini ya Nickel uliopo Musongati nchini Burundi unaokadiriwa kuwa na hifadhi ya tani milioni 150 za madini ya Nickel, Cobalt na Copper, na pia kuimarisha shughuli za kiuchumi za nchi hizo mbili.