Alhamisi , 14th Jan , 2016

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Rwanda nchini, Eugene Kayihura, ambapo amemuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Rwanda.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa

Akizungumza na Balozi Kayihura jana , ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu amemshukuru Balozi huyo kwa kumtembelea na ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano ulipo baina ya nchi hizi mbili.

“Nia yetu ni kushirikiana kwa pamoja kwa kuunganisha wafanyabiashara wetu, kwa kutumia Bandari ya Dar es salaam na reli ya kati, ambayo tutajenga kwa kiwango cha kisasa ‘standard gauge’ ili ziweze kubeba mizigo mingi na kwenda mwendo wa kasi” alisema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Balozi wa Rwanda, Kayihura amesema Tanzania na Rwanda ni nchi marafiki na zinafanyakazi wa pamoja, Rwanda iko tayari kushirikiana na Tanzania kikanda na kimataifa.

“Tunatumia Bandari ya Dar es salaam na Mombasa, tunashukuru kwa namna ambavyo mnaboresha Bandari ya Dar es Salaam, kwani Rwanda inafaidika pia kwa vile mizigo yetu mingi karibu asilimia 75 husafirishwa kupitia bandari hii” alisema Balozi Kayihura.