Ijumaa , 20th Jun , 2014

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani takwimu zinaonyesha watu wapatao milioni 43 duniani kote wamelazimika kuhama makazi yao kwa sababu ya vita na majanga ya asili.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Isaac Nantanga.

Takwimu hizo zimetolewa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Tanzania Bw. Isaac Nantanga ambapo amefafanua kuwa kwa sasa Tanzania ina takribani wakimbizi 65,084 wengi wao wakiwa ni kutoka Jamhuri ya Kidemkorasia ya Kongo.

Natanga ameeleza kuwa mpaka sasa idadi ya wakimbizi imepungua kutokana na kuimarika kwa hali ya usalama ndani ya nchi walizotoka. Pia serikali kupitia wizara hiyo imeweka jitihada za kulinda mipaka ya nchi kutokana na matukio ya kigaidi yanayozikumba nchi jirani.

Ameongeza kuwa mafanikio waliyopata mpaka sasa ni pamoja na kufungwa kwa kambi za wakimbizi zaidi ya kumi na mbili ambapo kambi ya mwisho kufungwa ni ya Mtabila wilayani Kasulu mkoani Kigoma iliyokuwa na zaidi ya wakimbizi 35,000.

Hata hivyo Bw. Nantanga amewataka wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la polisi au kwa serikali za mitaa kuhusiana na kuwepo na wageni wanaingia nchini kwa njia haramu.