TANAPA watoa neno, moto unaowaka Mlima Kilimanjaro

Jumatatu , 12th Oct , 2020

Kamishna Msaidizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa, (TANAPA), Pascal Shelutete, amesema kuwa moto uliozuka na kuanza kuteketeza sehemu ya hifadhi za Mlima Kilimanjaro, huenda wakafanikiwa kuuzima hii leo baada ya hapo jana kushindikana na kuendelea kuwaka usiku kucha.

Sehemu ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ikiteketea kwa moto.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 12, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio na kusema kuwa zoezi la kuuzima moto huo litakapokamilika shirika hilo litatoa tathmini ya hasara iliyojitokeza.

"Kama TANAPA tumefanya juhudi kubwa sana na asubuhi ya leo vikosi mbalimbali vimefika Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya zoezi hilo la kuuzima moto, na kazi ya kuuzima moto huo inaendelea na tunatarajia kwa nguvu hiyo iliyopelekwa moto huo utaweza kudhibitiwa kuzima kwa siku ya leo", amesema Shelutete.

Aidha ameongeza kuwa,"Bado tunaendelea kufanya tathmini na baadaye tutatoa taarifa kamili juu ya chanzo na madhara ambayo yamejitokeza, kipaumbele kwanza tunashughulikia masuala ya uzimaji wa moto halafu mengine yatafuata baadaye".

Moto huo ambao hadi sasa unaendelea kuteketeza sehemu ya Mlima Kilimanjaro ulizuka majira ya jumapili mchana ya Oktoba 11 mwaka huu na mpaka sasa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.