Jumatano , 27th Jan , 2021

Leo Januari 27, 2021, Rais Magufuli atazindua shamba la miti lililopo Butengo, Chato Geita, shamba ambalo linaelezwa kuwa mpaka sasa limeshatoa ajira mbalimbali kwa wakazi wa eneo hilo hali iliyopelekea kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Shamba la miti Chato

Miongoni mwa wananchi waliozungumza na EATV akiwemo Juliana Petro na Eliud Majeshi, wamesema kuwa kipato cha hela mwanzo kilikuwa ni kigumu lakini sasa hivi vijana wamenufaika kwa kwenda kufanya kazi katika shamba hilo na kupata fedha za kujikimu.

Shamba la miti la Chato lenye ukubwa wa hekta 69,000, lilianzishwa mwaka 2017 baada ya uharibifu mkubwa uliofanywa na wanachi kuvamia shamba hilo na ndipo serikali kupitia wakala wa misitu (TFS), wakaamua kuendeleza shamba hilo ili kutunza mazingira.

Imeelezwa kuwa shamba hilo ni la pili kwa ukubwa kati ya mashamba yanayomilikiwa na Serikali na limeanzishwa kama sehemu ya eneo la msitu mkubwa wa Hifadhi ya Biharamulo-Alabama, ni la pili kwa ukubwa baada ya Saohill.