Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu

Ijumaa , 1st Jan , 2021

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile, amesema kuwa Serikali itaweka mazingira wezeshi ya kuendeleza vijana wabunifu wa TEHAMA nchini.

Dkt. Faustine Ndugulile, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Dkt. Ndugulile, ameyasema hayo alipofanya ziara yake ya kutembelea Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Ndaki ya TEHAMA ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (COICT) zilizopo Dar es Salaam.

Amesema kuwa vijana wanabuni mifumo mbalimbali ya TEHAMA ya kutatua changamoto za wananchi ila wanakosa mazingira wezeshi ya kuendeleza na kukuza bunifu zao kama vile kupatiwa muda maalumu wa kuingiza sokoni bunifu zao kwa kufanya majaribio ya bunifu hizo kukubalika kwa wananchi, bila kulazimika kulipia gharama za usajili, kupata masoko, malipo ya kodi na leseni kuendana na matakwa ya uendeshaji wa kampuni na biashara nchini.

Amesisitiza kuwa azma ya serikali ni kuendeleza wabunifu wa TEHAMA ili waweze kutengeneza mifumo kuendana na mahitaji ya wananchi badala ya kuendelea kununua mifumo hiyo kwa gharama kubwa kutoka nje ya nchi ambapo serikali inatumia fedha nyingi kununua mifumo ya TEHAMA.

Amefafanua kuwa utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA hapa nchini, utaongeza wigo wa matumizi ya intaneti na huduma za mawasiliano na itajibu changamoto za wananchi na ametoa rai kwa Watanzania kujenga imani ya kutumia teknolojia rahisi zinazobuniwa na vijana wa ndani ya nchi bila kujali umri, uzoefu au majina ya kampuni zao.