Alhamisi , 26th Jun , 2014

Serikali ya Tanzania imeendelea kusisitiza kuwa imeondoa michango ya shule iliyokuwa ikichangiwa hapo awali isipokuwa kamati pamoja na bodi za shule zimepewa fursa ya kupanga michango ya shule zao inayohusu maendeleo kupitia vikao vyao.

Naibu waziri wa nchi, ofisi ya waziri mkuu TAMISEMI, Kassim Majaliwa.

Hayo yameelezwa leo, bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Elimu, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa ubungo, Mhe.John Mnyika aliyetaka kufahamu kauli ya serikali kuhusu michango inayoendelea kutozwa mashuleni.

Mhe Majaliwa amesema wameziagiza kamati pamoja na bodi za shule hizo kuzingatia hali ya kipato cha walezi na wazazi wa wanafunzi katika kupanga michango hiyo kupitia vikao vyao ili kuepukana na michango hiyo kuwa kero kwa wananchi.