Jumanne , 29th Sep , 2015

Serikali ya Tanzania imesaini mkataba wa shilingi milioni 240 kutoka nchi ya Polland kwaajili ya kusaidia uzalishaji wa pembejeo za kilimo pamoja na utekelezaji wa mradi wa maghala ya kuhifadhia chakula.

Waziri wa fedha nchini Tanzania Saada Mkuya Salum

Akizungumza baada ya kutia saini mkopo na makubaliano hayo waziri wa fedha nchini Tanzania Saada Mkuya Salum, amesema fedha hizo zimefika kwa wakati muafaka ambapo zitasaidia katika kuendeleza mradi wa utengenezaji wa matrekta ambayo yatatolewa kwa wakulima ili kuweza kusaidia kukuza na kuboresha shughuli za kilimo.

Bi. Mkuya amesema mbali makubaliano hayo waliyowekeana na serikali ya Polland fedha hizo zitasaidia katika ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula kutokana na kuwepo kwa uhaba wa maghala hayo nchini hivyo kusaidia kuhifadhi kiasi kikubwa cha chakula chenye kutosheleza katika soko la ndani na nje.

Kwa upande wake waziri wa Chakula na Ushirika Mh Steven Wassira amesema utekelezaji wa mradi huo utakapokamilika utasaidia kukuza kilimo pamoja na kutoa ajira kwa vijana ambao wamekuwa wakikwepa kujihusisha na shughuli za kilimo kutokana na kuwepo kwa vifaa duni katika uzalishaji wa mazao ikiwemo upungufu wa matrekta.

Wassira ameongeza kuwa mpaka sasa wakala wa uhifadhi wa Chakula NFRA ina uwezo wa kuhifadhi tani laki mbili pekee za chakula na kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuongeza kiasi cha chakula kinachohifadhiwa na kuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani laki nne kwa mwaka.