Jumanne , 2nd Feb , 2016

Mbunge wa jimbo la Kawe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Halima Mdee amesema serikali ya CCM imekwama katika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kutokana na kutoweka kipaumbele kwa miradi muhimu.

Mdee ameyasema hayo katika ukumbi wa bunge mjini Dodoma wakati akichangia katika kikao cha 6 cha Bunge la 11 linaloendelea mjini Dodoma.

''Mheshimiwa mwenyekiti miradi mingi imekwama kwa mfano mpango wa mwaka uliopita ulilenga kujenga barabara kilomita 5204 lakini zilizojengwa ni kilomita 2775 tuu ndizo zilizojengwa, pia kilimo kimekua kwa asilimia 3.4 ikimaanisha kimeshuka kutoka asilimia 6". Amesisitiza Halima Mdee.

Mbunge huyo ameitaka serikali kufikiri upya hasa katika vipaumbele vyake kwani asilimia 70 ya watanzania ni wakulima na wanaliingizia taifa asilimia 30 ya pato hivyo ni vyema serikali ikaangalia upya namna ya kuwawezesha kuweza kulima kwa tija na uwezekano wa kuuza mazao yao.

Aidha Halima pia amewakumbusha wabunge kwamba kama wabunge kazi yao ni kuisimamia serikali lazima waseme mafanikio na mapungufu ya serikali kupitia bunge ili serikali ijipange kutatua matatizo ya wananchi.