Jumatano , 18th Nov , 2015

Serikali imetakiwa kuendelea kujengea uwezo hospitali nchini hasa vitengo vya tiba ya mama na mtoto ili kuokoa maisha ya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati.

Baadhi ya watoto wachanga waliozaliwa Njiti katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam( PICHA NA MAKTABA)

Serikali imetakiwa kuendelea kujengea uwezo hospitali nchini hasa vitengo vya tiba ya mama na mtoto ili kuokoa maisha ya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati ambao huchangia theluthi moja ya vifo vya watoto nchini.

Hayo yamekuja katika siku ya mtoto njiti ambapo Hospitali ya Taifa Ya Muhimbili imepokea mashine tano zenye thamani ya shilingi milioni 15 kutoka kwa wahisani kwa ajili ya kuwasaidia watoto waliozaliwa kabla ya kutimia miezi yaani njiti kuweza kupumua kwa kipindi chote wanachosubiri kufikia muda wa kawaida wa kuzaliwa.

Akiongea wakati wa kupokea vifaa hivyo mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Said Meck Sadick amesema kuwa kuna upungufu mkubwa sana wa vifaa hivyo vya kupumulia katika hospitali nchini, hivyo wahisani wengine waige mfano huo kusaidia huduma mbalimbali katika hospitali zetu.

Kwa upande wake muuguzi katika Hospitali Ya Taifa Ya Muhimbili amesema zaidi ya watoto njiti 250,000 huzaliwa kila mwaka hapa nchini huku zaidi ya watoto elfu tisa wakipoteza maisha kila mwaka.

Akizungumzia sababu za kuwepo kwa watoto njiti mtaalam huyo amesema suala la umri mdogo, ukosefu wa vyakula vyenye virutubisho, upungufu wa damu.

Katika taarifa ya shirika la umoja wa mataifa la kusaidia watoto duniani (UNICEF) iliyotolewa hapo jana inaeleza kuwa nchini Tanzania, kila mwaka, watoto takribani 213,000 huzaliwa mapema sana kabla ya muda wao (watoto njiti) na zaidi ya 9,000 miongoni mwao hufariki kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa mapema.

Idadi hii ni takribani robo ya watoto wachanga 40,000 wanaofariki kila mwaka hapa nchini.

Vifo kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa kabla ya muda kutimia ni sababu kubwa ya pili inayosababisha vifo vya watoto wachanga hapa Tanzania.

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto. Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 166 kati ya 1,000 waliozaliwa hai mwaka 1990 hadi kufikia vifo 54 kati ya kila 1,000 waliozaliwa hai mwaka 2012.

Hata hivyo kasi ya kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa mwezi mmoja imekuwa ndogo, kutoka watoto 43 kati ya 1,000 waliozaliwa hai mwaka 1990 hadi watoto 21 kati ya 1,000 waliozaliwa hai mwaka 2012.

Pia kasi ya kupunguza vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na matatizo ya kuzaliwa njiti ni ndogo sana na hivyo basi vinaendelea kuchangia asilimia kubwa ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.