Jumanne , 11th Nov , 2014

Baraza la Wanawake Chadema, limemtaka mkuu wa jeshi la polisi nchini kuchukua hatua za haraka za kudhibiti mauaji ya kikatili na kinyama yanayoendelea katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa North Mara Wilayani Tarime.

Viongozi wa Baraza la Wanawake la Chama Cha Demokrasia Maendeleo nchini Tanzania, CHADEMA.

Katibu Mkuu Bawacha Bi. Kunji Yusuf amesema hayo wakati akihutubia wananchi wa Manispaa ya Musoma ambapo amesema baadhi ya askari hao wa jeshi la polisi wamekuwa wakikiuka maadili ya kazi hiyo kwa kuendesha vitendo vya mauaji, unyanyasaji na ukatili mkubwa dhidi ya wananchi lakini hadi sasa hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa katika kurejesha amani katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mstaafu wa BAVICHA Bw. John Heche, amesema CHADEMA, itaendelea kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kutoa elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa ili kuwawezesha wananchi kutoa uamuzi sahihi wakati ukifika.

Aidha Mwenyekiti wa Vijana wa Chama hicho amewataka wananchi kuzisoma rasimu zote mbili kati ya rasimu ya pili ya Katiba yenye maoni yao pamoja na Katiba Inayopendekezwa ili wasifanye makosa itakapofikia kwenye upigaji wa kura ya Maoni.