Sababu ya Rais wa Msumbiji kuja nchini yatajwa

Jumatatu , 11th Jan , 2021

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, atawasili nchini hii leo Januari 11, 2021, katika ziara yake ya siku mbili wilayani Chato yenye lengo la kudumisha undugu baina ya nchi ya Tanzania na Msumbiji.

Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi, na kusema kuwa ziara hiyo ina umuhimu mkubwa katika masuala ya kiuchumi na kwani hadi sasa kuna makampuni makubwa kutoka Tanzania yamewekeza mtaji mkubwa nchini Msumbiji.

"Ni ziara ya kindugu ambayo ilipangwa kufanyika muda mrefu mwaka jana, lakini haikuweza kufanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchaguzi mkuu, mahusiano ya kihistoria, kidplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizi mbili yameendelea kuimarika", amesema Waziri Kabudi.

Aidha Waziri Kabudi ameongeza kuwa, "Viongozi wetu watabadilishana mawazo ya namna ya kuendeleza na kuwezesha ufanyaji wa biashara lakini pia kuongeza uwekezaji wa Watanzania ndani ya Msumbiji na watu wa Msumbiji ndani ya Tanzania".