RC Kilimanjaro alia na TANESCO 'Toeni taarifa'

Jumatatu , 25th Jan , 2021

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amelitaka Shirika la umeme nchini (TANESCO), kuhakikisha wanatoa taarifa mapema kabla hawajakata umeme ili isiweze kuleta madhara kwa wananchi na wafanyabishara wakubwa.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 25, 2021, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, ambapo amesimulia ni kwa jinsi gani mteja aliyekuwa analipa milioni 100 kila mwezi kama bili ya umeme, alivyoharibikiwa na mtambo wake wa kutengeneza nondo baada ya umeme kukatika.

"Nina mfanyabiashara ambaye anazalisha chuma alikuwa keshafika mbali sana, siku moja amechoma chuma chake cha kutengeneza nondo na amenunua kinu cha fedha nyingi, chuma kile kimeshayeyuka anataka sasa aanze kutengeneza nondo umeme ukakatika,  kile chuma kikawa jiwe, kinu kikafa, kipindi hicho alikuwa analipa bili ya umeme ya milioni 100 kila mwezi", amesema RC Mghwira

Aidha RC Mghwira ameongeza kuwa, "Hata kama tunazalisha umeme kidogo, TANESCO watupe taarifa, mfano mimi Meneja akinitumia message ya hitilafu na ikifika tu nawasambazia wananchi wangu, wakuu wa wilaya na wenyewe nawaambia sambazeni, nina orodha ya wazalishaji wetu wakubwa wote nawaambia jamani kutakuwa na hitilafu ya umeme"