Alhamisi , 5th Mei , 2016

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daud Ntibenda amemsimamisha kazi Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Peter Mikimba, kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daud Ntibenda

Ntibenda ametoa uamuzi wa kumsimamisha kazi, Mhandisi huyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema Mhandisi Mikimba anakabiliwa na tuhuma za kushindwa kusimamia miradi ya ujenzi wa Maabara, ujenzi na ukarabati wa barabara za wilaya.

Pia amesema ameshindwa kusimamia ujenzi wa nyumba za walimu kwa mwaka wa fedha 2013/14, ambapo athari zake zimejitokeza hivi karibuni katika miradi hiyo.

Aidha Ntibenda amemwagiza Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega kuunda tume itakayochunguza tuhuma zinazomkabili Mhandisi Mikimba, kuanzia Mei 4 mwaka huu hadi Mei 15/2016 na kuamuru kwa muda huo tume hiyo iwe imeshakamilisha uchunguzi wake.

Ametoa wito kwa watendaji wote wa serikali Mkoani hapa, kusimamia kwa makini na weledi miradi yote inayotekelezwa na serikali kwa wananchi ili iwe na tija.