Aliyekuwa Mkurugenzi Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC, Julius Mallaba.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mabadiliko ya Utendaji katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kumteua Ndugu Kailima Ramadhani Kombwey kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Aidha, Rais Kikwete amemteua Jaji Richard Mziray kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vile vile, Rais Kikwete amewateua majaji wapya 13 wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumamosi, Julai 25, 2015 na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue mjini Dar es Salaam inasema kuwa teuzi hizo zote zimeanza leo hii.
Kwa mujibu wa taarifa ya Balozi Sefue, Ndugu Kombwey ambaye anaapishwa baadaye leo jioni, anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndugu Julius Benedicto Mallaba.
Badala yake, Rais Kikwete amemteua Bwana Mallaba kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Kombwey alikuwa Mkurugenzi wa Utawala, Tume ya Uchaguzi.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa Jaji Mziray ambaye anateuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam.
Majaji wa Mahakama Kuu ambao wameteuliwa na Rais Kikwete, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ndugu Ignas Pius Kitusi ambaye ni Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Ndugu Wilfred Peter Dyansobera ambaye ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu; Ndugu Lameck Michael Mlacha ambaye ni Naibu Msajili na Mwenyekiti wa Baraza la Rufani la Kodi; Ndugu Salima Mussa Chikoyo ambaye ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi; Ndugu Isaya Arufani ambaye ni Naibu Msajili na Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania na Ndugu Julius Benedicto Mallaba.
Wengine ni Ndugu Adam Juma Mambi ambaye ni Katibu Msaidizi, Tume ya Kurekebisha Sheria; Ndugu Sirilius Betran Matupa ambaye kwa sasa ni Msaidizi wa Rais, Sheria, Ofisi ya Rais, Ikulu; Ndugu Issa Maige ambaye ni wakili wa kujitegemea, Ndugu Licia Gamunya Kairo ambaye ni wakili wa kujitegemea; Dkt. Masoud Shaaban Benhaji wakili wa kujitegemea na Mhadhiri Mwadamizi, Chuo Kikuu Huria, Dar es Salaam, Ndugu Victoria Makani ambaye ni wakili wa kujitegemea na Ndugu Rehema Joseph Kerefu ambaye ni mwanasheria wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Taarifa hiyo imesema kuwa wakati Ndugu Kombwey anaapishwa leo, majaji wataapishwa katika tarehe itakayotangazwa baadaye.