Jumanne , 14th Feb , 2017

Idara ya Uhamiaji Kanda ya Dar es Salaam, imewataka raia 7 wa China kuondoka nchini kutokana na kukiuka taratibu sheria za ukazi, huku raia mmoja wa Uganda akishikiliwa kwa kuwa na hati 15 za kusafiria za Burundi na Madagascar kinyume cha Sheria

Kamishna John Msumule

 

Kamishna wa Uhamiaji Kanda ya Dar es Salaam, John Msumule, amewaambia waandishi wa habari kuwa, mbali na raia hao wa China pia wanawashikilia raia wengine 25 wenye asili ya ki-Asia kwa kufanya kazi nchini kinyume cha sheria na kwamba watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili wao pamoja na waajiri wao.

Aidha, Kamishna Msumule amesema, wanawashikilia waajiri wawili kwa kosa la kuwatumikisha raia wa kingeni bila kibali na kuwataka waajiri kote nchini kuhakikisha wanafuata taratibu za uajiri kabla ya kuingiza raia wa kigeni kwani idara hiyo haitawafumbia macho.

Katika hatua nyingine Kamishna Msumule amesema wanapanga kuwataja hadharani maafisa wa idara hiyo ambao wamekuwa siyo waminifu wakishirikiana na wahamiaji haramu kughushi nyaraka za ukazi na vibali vya kazi kwa lengo la kuongeza uwajibikaji katika idara hiyo.