Jumanne , 14th Jun , 2016

Wafanyabiashara wanaoweka na kutoa fedha zao kwenye benki mbali mbali nchini wametakiwa kutumia mfumo wa malipo kwa njia za kielektroniki ikiwemo ile ya mitandao ya simu za mkononi ili kuepusha uwezekano wa kuporwa fedha zao na majambazi.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Siro

Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Siro, ametoa wito huo jijini Dar es Salaam leo na kwamba matukio ya ujambazi yanayotokea sehemu kadhaa ya jiji yanatokana na watu kubeba na kutunza pesa zao kiholela.

“Watanzania sasa tuachane na tabia za zamani ya kwamba pale unapokuwa na pesa nyingi basi unataka kila mtu afahamu...hiyo ni hatari sana kwa usalama kwani pesa ni adimu na kila mtu anaitafuta na unaweza kujikuta ukivamiwa na majambazi na kuuwawa,” ametahadharisha kamanda Siro.

Kwa mujibu wa Kamanda Siro, jeshi la polisi limeimarisha ulinzi katika benki na taasisi mbali mbali za fedha na kwamba kinachotakiwa ni kwa wamiliki kuzingatia kanuni za usalama za utunzaji wa pesa zao.

“Sasa hivi kuna maendeleo makubwa ya teknolojia hasa namna mtu anavyoweza kutuma na kupokea pesa....tuanze sasa kutumia teknolojia ya kupokea na kutuma pesa kwa njia ya mtandao ili kuepusha kubeba kiasi kikubwa cha pesa,” amesema Kamanda Siro na kuonya kuwa “Hebu fikiria una pesa nyingi lakini kutokana na uzembe unapigwa risasi na kuuwawa na kuwaacha watoto na familia yako ikihangaika.....tujenge tabia ya kuwa na usiri pale tunapobeba pesa nyingi,”