Jumamosi , 27th Aug , 2016

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeongeza nguvu kwa kutuma askari wengine 80 katika oparesheni ya kusaka majambazi inayoendelea katika maeneo ya Vikindu, wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Kamishna Simon Sirro

Akizungumza na vyombo vya habari leo katika kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo Kamishna Simon Sirro, amesema Jeshi hilo limeanza rasmi oparesheni hiyo usiku wa kuamkia jana, ikiwa na lengo kusaka watu wanaoshukiwa kuwa ni majambazi wanaodaiwa kufanya matukio kadhaa ya ujambazi likiwemo lile la kuuawa kwa askari wanne waliokuwa wakienda lindoni, katika benk ya CRDB, Mbade jiji Dar es Salaam.

Amesema kuwa katika oparesheni hiyo kuna watu waliouawa na wengine wanashikiliwa na jeshi hilo, lakini amekataa kutaja idadi yoyote ile ya waliouawa au waliokamatwa kwa sababu za kiusalama kwa kuwa oparesheni hiyo bado inaendelea.

“Raia wametupa taarifa na tunazifanyia kazi, oparesheni ni kwasiku mbili sasa na bado tumetuma wengine zaidi ya 80 na ni mapambano ya kawaida kwetu polisi hata kama polisi akifariki ni kawaida, lakini taarifa itawajia siku ya Jumanne” amesema

Kuhusu taarifa za uwepo wa askari aliyeuawa, Kamishna Sirro amekataa kuthibitisha au kukanusha na kusema kuwa taarifa kamili kuhusu oparesheni hiyo itatolewa siku ya Jumanne ya wiki ijayo.

Amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu, na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kutoa taarifa zitakazoweza kufichua wahalifu hao na kusisitiza kuwa jeshi hilo litawabaini na kuwatia nguvuni wote waliohusika.

Katika hatua nyingine, Sirro ameendelea kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote yale katika mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya zuio la jeshi la polisi la kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na maandamano nchi nzima.

“Kuna vijana wanapewa pesa shilingi elfu 40 kwa ajili ya kufanya maandamano na viongozi wasiolitakia mema taifa hili, kijana ajiulize hizo elfu arobaini zitamsaidia nini endapo atavunjwa mguu kwa kushiriki maandamano hayo” amesema.

Usiku wa kuamkia jana, hali ya taharuki iliwakumba wakazi wa Vikindu baada ya kikosi maalum cha askari kuvamia nyumba moja iliyoko eneo hilo, na kisha kuzuka kwa majibizano ya risasi kati ya polisi na wanaodaiwa kuwa ni majambazi waliokuwa katika nyumba hiyo.