Jumanne , 12th Apr , 2016

Kamanda wa Polisi kanda Maalum ya Dar es salaam Simon Sirro amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa kuhakikisha wanawachukua watoto wa mitaani na ombaomba waliozagaa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.

Kamanda wa Polisi kanda Maalum ya Dar es salaam Simon Sirro amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa kuhakikisha wanawachukua watoto wa mitaani na ombaomba waliozagaa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na kuwapeleka katika vituo vinavyotoa huduma kwa makundi hayo.

Kamanda Sirro ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari na kuongeza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaoomba katika maeneo ya jiji hali inayotishia ulinzi na usalama, hivyo serikali imeamua kukomesha tabia hiyo na wale wenye mahitaji maalum wanatakiwa kupelekwa kwenye vituo ambavyo vinatoa huduma.

Oparesheni maalum ya kuondoa ombaomba katika maeneo ya jiji la Dar es salaam inatarajiwa kuanza Jumatatu wiki ijayo ambapo ombaomba wote watakaopatikana katika maeneo ya barabarani watakamatwa na kuondolewa katika maeneo hayo.

Aidha Kamanda sirro amepiga marufuku vikundi vyote vya ulinzi shirikishi ambavyo havijaanzishwa kwa kufuata sheria kwani sheria inataka kikundi shirikishi kianzishwe chini ya serikali ya mtaa na kifanye shughuli zake ndani ya mtaa husika kinyume na hapo amewaita kuwa ni waganga njaa na popote watakapokutwa watafikishwa kituo cha polisi.

Msikilize hapa;-

Sauti ya Kamanda wa Polisi Dar es salaam