Jumatano , 28th Sep , 2022

Mkuu wa mkoa wa Tanga Omari Mgumba, amewataka vijana waliohitimu mafunzo ya operesheni Jenerali Venance Mabeyo 2022 wanaokwenda kujiunga na vyuo vikuu, kutumia vizuri mitandao ya kijamii badala ya kuweka picha za utupu ambazo zimekuwa zikiwadhalilisha na kuleta fedheha kwa Taifa.

Mkuu wa mkoa wa Tanga Omary Mgumba, akikagua vijana wanaomaliza mafunzo

Mgumba ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo katika kambi ya JKT Kabuku 835 KJ wilayani Handeni mkoani Tanga, ambapo alisema vijana wengi waliopo vyuoni wamekuwa na uhuru uliopitiliza na kufanya mambo bila uwepo wa usimamizi.

"Niwasihi wazazi wenzangu muwe mnafanya kuwatembelea watoto wenu wanapokuwa vyuoni, lakini wahitimu leo niwaase mkatumie vizuri mitandao ya kijamii kwa ajili ya faida na sio vinginevyo maana vijana wengine waliopo vyuoni wanaweza kudanganywa kwenye mitandao ya kijamii ukashurutishwa jambo ambalo unaweza kufanya kwa tamaa,"amesema RC Mgumba

Mkuu huyo wa mkoa huyo amesema matokeo yake wanadhalilisha wazee wao, jamii na ndugu na Taifa kwa ujumla hivyo hakikisheni suala la nidhamu mnalishikilia kweli hasa wale wanaoenda kuishi vyuoni.