"Nimeacha nafasi za ACT Wazalendo"- Dkt. Mwinyi

Alhamisi , 19th Nov , 2020

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi, ametangaza baraza jipya la Mawaziri katika Serikali yake huku akiacha kutangaza majina ya Mawaziri katika Wizara mbili na kusema kuwa ma Naibu Waziri atawachagua itakapobidi.

Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi.

Awali akizungumza hii leo Novemba 19, 2020, Ikulu ya Zanzibar, Rais Mwinyi amesema kuwa kuna baadhi ya wizara amezibadilisha ikiwemo kuongeza idadi ya mawaziri katika Ofisi ya Rais kutoka idadi ya mawaziri watatu ilivyokuwa awali na kuwa na mawaziri wanne, huku akisisitiza suala la wazanzibar kuwa wamoja.

"Baada ya kukamilika kwa uchaguzi na ACT Wazalendo, kupata zaidi ya asilimia 10, tuliwaandikia barua ili walete jina la Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kuwa jina bado halijafika lazima tuache wazi, nimeacha nafasi mbili za mawaziri wa chama cha ACT Wazalendo endapo watakuwa tayari lakini mpaka leo hawajaenda kusajiliwa na lazima tuwape muda wa kikatiba", amesema Rais Dkt. Mwinyi.

Aidha Dkt Mwinyi akizungumzia suala la kukutana na kufanya maridhiano na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT wazalendo, amesema kuwa yeye tayari amekwishafanya yale yote ambayo katiba inawataka kufanya na kwamba maamuzi yaliyobaki ni kwa chama hicho.