Jumanne , 15th Sep , 2020

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, amesema kuwa licha ya kwamba chanzo cha moto ulioteketeza bweni la Shule ya Byamungu Islamic hakijajulikana, lakini bado wanatafuta vyanzo vingine na kudai kuwa huenda kuna adui mwingine aliyesababisha maafa hayo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro

IGP Sirro ametoa kauli hiyo alipofika kwenye eneo la tukio la moto ulioteketeza bweni la shule hiyo, na kuongeza kuwa hata mifumo ya umeme katika jengo hilo haikuwa mizuri pamoja na jengo lenyewe halikuwa madhubuti na kwamba uchunguzi bado unaendelea.

"Jengo lenyewe sijui hata Afisa Elimu na wakaguzi walikuwa wanajua watoto wanalala kwenye hili jengo, tunajaribu kutafuta vyanzo vingine inawezekana jengo halikuwa madhubuti, lakini inaweszekana kuna adaui wa nje amechukua huo mwanya kufanya uhalifu", amesema IGP Sirro.

"Tutafanya upelelezi wa kina na tutapata majibu, niwahakikishie tukipata taarifa sahihi tutawashughulikia kweli kweli, hatuna mchezo na mtu ambaye kwa uzembe wake au nia yake ovu anasababisha vifo, niliwahi kusema damu ya Mtanzania huwa haiendi hovyo, akishakufa Mtanzania lazima aliyesababisha tumshughulikie kwa mujibu wa taratibu", ameongeza IGP Sirro.

Tukio la ajali ya moto katika shule ya Byamungu Islamic iliyoko wilayani Kyerwa mkoani Kagera, lilitokea usiku wa kuamkia jana Septemba 14, 2020, na kupelekea vifo vya watoto 10 na wengine 7 kujeruhiwa, ambapo bweni hilo lilikuwa na wanafunzi 74.