Jumatano , 8th Jul , 2015

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania NEC, imesema imefikia nusu ya lengo la kuandikisha watanzania milioni 22 au 23 ambapo mpaka kufikia jana tume imekwisha andikisha zaidi ya wapiga kura milioni 11.

Mwenyekiti wa NEC,Jaji Mstaafu Damian Lubuva

Akizungumza Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani alipojiandikisha Rais Jakaya Kikwete mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema mpaka sasa mikoa 13 imeshakamilisha kazi kuandikisha na takribani wapiga kura milioni 11,248 194 wameshasajiliwa.

Amesema kwa sasa wanaendelea kuandikisha katika mikoa 11 na kwa mkoa wa Dar es Salaam Zoezi hilo litaanza rasmi kuanzia Julai 16 na Zanzibar wataanza Julai 13 mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kujiandikisha Rais Kikwete alisisitiza wananchi wajitokeze kujiandikisha ili waweze kupata haki yao ya msingi ya kuweza kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayemtaka

Aidha Rais Kikwete alipongeza tume ya uchaguzi kwa kazi nzuri waliyoifanya na ya kurudhisha ya kuandikisha watanzania kwenye Daftari hilo licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa.