Alhamisi , 2nd Jun , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa hatua anazozichukua katika uboreshaji wa sekta ya Elimu ni kwa ajili ya Maendeleo ya nchi na Watanzania kwa Ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam wakati wa Hafla ya kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Maktaba mpya na ya kisasa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema imefika wakati ni lazima watu wabadilike ili kuendana na kasi ya maendeleo ya kweli yanayo takiwa na kila Mtanzania.

Rais Magufuli amesema kuwa watumishi na Watanzania wanapaswa kuzingatia sheria za nchi ili kuleta maendeleo chanya ikiwemo kupata wasomi wenye vigezo stahiki ambao watalalileta taifa maendeleo.

Rais Magufuli amesema serikali yake imejidhatiti katika kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa wakati na kwa wanafunzi wanaostahili ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kusomea kwa kuongeza mabweni ya wanafunzi wengi zaidi.

Aidha Dkt. Magufuli amesema kwa kuwa anajua adha wanazoipata wanafunzi wanakaa nje ya vyuo kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ataenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya Ujenzi wa Mabweni chuoni hapo kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri zaidi ya kusomea.