Jumatano , 3rd Feb , 2021

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme, amekataa kukabidhi madawati 50 pamoja na meza 10 za walimu katika shule ya msingi Mtakanini iliyopo wilaya ya Namtumbo  mkoani humo baada ya kukuta meza pamoja na madawati yakiwa mabovu na kuagiza yaende yakafanyiwe marekebisho.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme

Hatua hiyo imejiri wakati alipokwenda kuzindua vyumba viwili vya madarasa pamoja na kukabidhi madawati 50 na meza 10 za waalimu katika shule ya Mtakanini iliyopo mkoani humo.

"Madawati yameshavimba tayari hata mtoto hajakalia, meza imeachia, kiti kimeachia wakikaa sketi zitachanika naomba marekebisho yakafanyike, Haya madawati wala meza sikabidhi mpaka zikafanyiwe marakebisho, siwezi kukabidhi kitu kibovu namna hiyo, hawezi kututengeneza kitu kibovu cha namna hii, mimi na akili zangu timamu nakabidhi kitu kibaya namna hii siwezi", amesema RC Mndeme

Awali akielezea changamoto ambazo zinaikabili shule hiyo, mkuu wa wilaya ya Namtumbo Sophia Kizigo, amesema shule hiyo inakumbwa na changamoto ya ukosefu wa madawati 40 pamoja na meza za walimu hali inayofanya wanafunzi kushindwa kushiriki masomo kikamilifu.