Jumanne , 17th Mei , 2022

Jeshi la polisi mkoani Iringa linamshikilia Mkurugenzi wa shule ya Sun Academy, Nguvu Chengula, kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi Alifa Mkwawa, ambaye ni mzazi, kwa kutumia kitako cha bastola baada ya kuombwa uhamisho wa mtoto anayesoma katika shule hiyo.

Alifa Mkwawa, Mzazi aliyepigwa na kitako cha Bastola

Kamanda wa Polisi mkoani humo Allan Bukumbi, amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 6:00 mchana maeneo ya shule hiyo iliyopo mtaa wa Mawelewele ambapo chanzo cha tukio hilo ni mzozo uliotokana na mtuhumiwa kugoma kutoa uhamisho wa mtoto wa mlalamikaji kwa kile kinachodaiwa kuwa hajalipa ada ya mtoto huyo.

Katika hatua nyingine jeshi hilo kwa nyakati tofauti limefanikiwa kukamata watuhumiwa watano na kuharibu mashamba matatu ya bangi iliyolimwa kwa mchanganyiko wa mahindi na maharage katika Kata ya Image wilayani Kilolo ambapo wakulima hao wanatumia mbinu ya kulima vishamba vidogo vidogo mtawanyiko na kupanda bangi kati ya mashina 20 hadi 60 kwenye maeneo ya misitu na makorongoni.