Mwinyi mgeni rasmi sherehe za Mapinduzi Zanzibar

Jumapili , 10th Jan , 2021

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 57 za Mapinduzi ya Zanzibar ambazo kwa mwaka huu zitafanyika katika viwanja vya mnazi mmoja mkoa wa Mjini Magharibi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustafa amesema sherehe hizo zitaambatana na maandamano ya mapinduzi yatakayo washirikisha vijana kutoka Unguja na Pemba ambayo yataanzia katika uwanja wa Matumbaku  hadi uwanja wa Mnazi mmoja , ambapo Rais atapokea maandamano hayo pamoja na maonyesho ya vikosi vya ulinzi na usalama.

"Katika sherehe hizo viongozi mbalimbali watahudhuria wakiwemo wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, viongozi wa vyama vya siasa, mabalozi wa nchi za nje waliopo nchini pamoja na wananchi wa mikoa mitano ya unguja na pemba" amesema

Kitwana amesema sherehe za mwaka huu zitakuwa za kwanza tokea serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dkt Husein Mwinyi iingie madarakani mwezi novemba mwaka 2020, hivyo amewataka wananchi kuhudhuria kwa wingi katika sherehe hizo ili kumuunga mkono Rais wa Zanzibar pamoja na serikali yake.

Kitwana ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa huo  amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri ili kuhakikisha hali ya amani inaimarika wakati wote wa sherehe hizo.

Aidha Kitwana amewaomba wananchi wote kuhudhuria kwa wingi katika viwanja vya maisara usiku wa januari 11 kwa ajili ya kuangalia fashfash za maadhimisho ya sherehe za miaka 57 ya mapinduzi ya Zanzibar ambapo mgeni rasmi siku hiyo anatarajiwa kuwa Makamo wa pili wa rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdalla.