Jumanne , 9th Feb , 2016

Mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyotokea katika kijiji cha Kigurukwa, wilayani Mvomero mkoani Morogoro yamesababisha mauaji ya mbuzi 75 waliokatwakatwa kwa mapanga.

Tukio hilo lililotokea leo, limemlazimu Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo Mh Mwigulu Nchemba kufika katika eneo hilo bila kuchelewa na kuchukua hatua.

Mara baada ya kuwasili na kushuhudia hali halisi huku mbuzi zaidi ya 75 wakiwa wamekufa, Mh. Mwigulu ameagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya kuhakikisha waliofanya uharibifu huo wanakamatwa mara moja.

Pili ameagiza kupitia hukumu ya mahakama iliyotolewa mwaka 2015 kuweka mipaka kati ya eneo la wakulima na wafugaji itekelezwe haraka iwezekanavyo.

Mwisho waziri Mwigulu Nchemba ameagiza kuwepo mkutano wa hadhara wa wakulima na wafugaji na viongozi wote wa serikali wa wilaya na mkoa tarehe 20/02/2016 ndani ya kata ya Hembeti.