Alhamisi , 31st Dec , 2020

Taharuki imeibuka kwa wakazi wa kitongoji cha Iyula A katika kata Iyula, wilayani Mbozi, baada ya mwanamke mmoja Mariam Mligo (19) anayedaiwa kuwa mjamzito wa miezi tisa, ujauzito wake kupotea katika mazingira tata muda mfupi baada ya kushikwa na uchungu.

Mwanamke mjamzito

Tukio hilo lililozua taharuki kubwa katika Kata ya Iyula, ambapo mama huyo awali alipaswa kujifungua Desemba 25, 2020, na baadaye mama huyo kujikuta hana ujauzito.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Iyula A, Mawazo Mwamlima, amesema kuwa tukio hilo limesababisha taharuki na sintofahamu kwa wakazi wa kitongoji hicho kwa kuwa si tukio la kawaida na kwamba hata mara baada ya kumpeleka hospitali hakuonesha dalili yoyote ya kwamba labda amejifungua.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Mbozi, Dkt. Mponjoli Mwangosi, amethibitisha kumpokea mwanamke huyo katika kituo hicho cha Afya Iyula akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa, ambapo uchunguzi wa awali ulionesha kuwa mama huyo hakuwa na ujauzito.

Aidha Dkt. Mponjoli ameongeza kuwa hali hiyo ipo kwenye mambo ya uzazi kwa akina mama na kuna kitu kinaitwa mimba isiyo halisia ‘Pseudocyesis Pregnance”, hali hiyo huwaingiza watu wengi kwenye migogoro ya ndoa na kuibua taharuki wakisema kuna mambo ya kishirikina, hali hii ambayo hutokana na magonjwa ya wanawake.