Jumamosi , 6th Dec , 2014

Wananchi wa vijiji vya Igowole na Mufindi Kibaoni wilayani Mufindi wameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya Nyololo Igowole hadi Mgololo yenye urefu wa kilomita 77.6

Wananchi wa vijiji vya Igowole na Mufindi Kibaoni wilayani Mufindi wameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya Nyololo Igowole hadi Mgololo yenye urefu wa kilomita 77.6 kwani barabara hiyo ni muhimili kwa uchumi wa wilaya ya mufindi na taifa kwa ujumla kutokana na uwepo wa viwanda vikubwa kikiwemo kiwanda cha karatasi cha mgololo.

Wananchi hao wamesema hayo kwenye mikutano ya hadhara iliyofanywa na Naibu Waziri wa Ujenzi mhandisi Gerson Lwenge wakati alipotembelea kukagua barabara na kuongea na wananchi wa vijiji vinavyopitiwa na barabara hiyo ambapo wananchi hao wamemwambia Naibu Waziri huyo kuwa wamekuwa wakiahidiwa kujengewa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa muda mrefu sasa lakini utekelezaji wake umekuwa kitendawili.

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi katika kijiji cha Kibaoni bwana Jacob Sanga amesema ahadi za serikali zisizoambatana na utekelezaji kujenga barabara  hiyo zinakweka chama hicho tawala katika wakati mgumu ambapo wao kama viongozi wamekosa majibu ya kuwapa wananchi wanapohoji utekelezwaji wa ahadi hiyo ya serikali.

Akijibu malalamiko hayo Naibu Waziri wa Ujenzi Gerson Lwenge amesema serikali imeshaanza hatua za ujenzi wa barabara hiyo kwa kufanya upembuzi yakinifu hivyo kuwatoa hofu wananchi hao na kwamba serikali ina thamini mchango unaotolewa viwanda vya chai, kahawa na karatasi vinavyotegemea barabara hiyo kwa ajili ya kusafirisha malighafi pamoja na bidhaa zinazotoka viwandani humo.