Ijumaa , 20th Nov , 2020

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni imempandisha kizimbani, Alphonce Gerald, akikabiliwa na shtaka la kujaribu kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka nane.

Gerald (30), ambaye ni Mkazi wa Chanika Dar es Salaam, amefikishwa  Mahakamani hapo na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu  Silayo.

Akisoma shtaka hilo, mwendesha mashtaka wa umma, ASP Hamis Said, amedai kuwa Oktoba 26, 2020  eneo la Kigogo Mburahati, Dar es Salaam, mshtakiwa alijaribu kumlawiti mtoto huyo (jina limehifadhiwa).

Baada ya kusomewa shitaka hilo mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka umedai upelelezi umekamilika, hivyo umeomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa hoja za awali(Ph).

Hakimu Silayo, alitoa masharti ya dhamana kuwa mshtakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho na kitambulisho cha Taifa, watakaotia saini dhamana ya milioni mbili  kwa kila mdhamini.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameshindwa kutimiza masharti, hivyo alirudishwa rumande hadi Desemba 2, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.