Mlinzi wa Meja Jenerali Mstaafu akamatwa

Wednesday , 13th Sep , 2017

Jeshi la Polisi linamshikilia mlinzi wa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mirataba na mfanyakazi mmoja wa benki kwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika kupanga njama za shambulizi la Meja huyo lililotokea nyumbani kwake Ununio siku za hivi karibun

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, Lazaro Mambosasa.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa wakati alipokuwa anaongea na waandishi wa habari na kusema kwa mujibu wa muhusika amewaeleza kwamba majira ya mchana huwa analinda peke yake lindo hilo huku akiwa na silaha aina ya shortgun.

"Katika mazingira ya kushangaza mlinzi huyo aliweka silaha kinyume kabisa na maadili ya utunzanji wa silaha maana aliiweka juu ya kitanda, halafu akatoka mikono mitupu kwenda kuwapa ushirikiano waliyofanya uhalifu huo kwa kuwafungulia mlango na kutenda uhalifu", amesema Mambosasa.

Pamoja na hayo, Kamanda Mambosasa ameendelea kwa kusema "Alitueleza kwamba aliamriwa akimbie naye akatii bila ya shuruti lakini silaha yake akaiacha pale pale alipokuwa ameiacha awali na kurudi baadae, askari huyu ambaye tuna uhakika amepitia mafunzo ya JKT angekuwa askari kweli wa kuhakikisha usalama wa maeneo anayoyalinda asingeenda kufungua geti bila ya kuwa na silaha. Kwa hiyo mashaka hayo ya msingi yametufanya tumkamate kwa kuwa aliiacha silaha na kutopigwa kofi au kwenzi na hao wahalifu".

Kwa upande mwingine, Kamanda Mambosasa amesema wamemkamata mmoja wa wafanyakazi wa benki ambaye anadai alikuwa anawasiliana na mtu wa nje ya ofisi ili aweze kumfuatilia Meja Jenerali Vicent wakati alipotoka kuchukua fedha benki.