Mkutano kati ya jimbo na nchi unamaanisha nini?

Jumapili , 18th Oct , 2020

Leo tarehe 18,Oktoba Ubalozi wa Tanzania, nchini China kupitia ukurasa wake wa twiter umeandika kuhusiana na mkutano wa biashara kati ya Tanzania na Jimbo la Henan la nchini China utakaofanyika mwezi Novemba 2020 kwa njia ya mtandao.

Kushoto ni picha ya sehemu ya Jiji la Dar es Salaam, kulia ni sehemu ya picha ya Jimbo la Henan.

Kupitia mkutano huo fursa za kuuza bidhaa za Tanzania katika soko la Henan zitawasilishwa na kujadiliwa zaidi.

Katika mkutano huo taasisi ya China Council for the Promotion of International Trade Henan SubCouncil, ndiyo itakuwa jukwaa na daraja mama katika kufungua mlango wa jimbo hilo kwa bidhaa za Tanzania.

''Makubaliano hayo yamefikiwa leo jijini Zhengzhou katika Mkutano wa Balozi wa Tanzania,Nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki, na Mwenyekiti wa China Council for the Promotion of International Trade Henan Sub Council,  Liang Jieyi," ulieleza ukurasa huo Tanzania Embassy in China.

Fursa ambazo nchi ya Tanzania itanufaika nazo ni pamoja na soko la malighafi na bidhaa zitokanazo na kilimo na uvuvi, fursa za utalii kutokana na jimbo hili kuwa na zaidi ya watu milion 90 ikiwa ni  idadi kubwa dhidi ya Tanzania na Kenya pia soko la vito vya thamani na vile vya kiutamaduni.

Aidha jimbo la  Henan ni la tatu nchini humo kuwa na idadi kubwa ya watu ambao ni milioni 95 likiwa na ukubwa wa km za mraba 167,000. Uchumi wa Jimbo hilo unategemea sekta ya Viwanda na kilimo.

Jimbo hilo linaongoza kwa uzalishaji wa ngano na mwaka jana GDP ya Henan ilifikia Dola za Kimarekani bilioni 725 huku Tanzania ikiwa Dola bilioni 63.18