Alhamisi , 31st Dec , 2020

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, Fabian Manoza, ameagiza kukamatwa na kuwekwa ndani wenyeviti wa vitongoji 8, katika Kata ya Itinje wilayani humo, wanaodaiwa kula fedha za michango ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya Kata hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, Fabian Manoza.

Mkurugenzi huyo ametoa amri ya kukamatwa kwa viongozi hao wa serikali za mitaa, kwenye ziara yake ya kukagua na kuhamasisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, iliyoshirikisha kamati ya ulinzi na usalama pamoja na kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapo na kujionea kukwama kwa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya sekondari ya Kata ya Itinje.

"Hapa kuna mambo makubwa mawili ikiwemo ya hawa wenzetu waliokula hela zetu na hawataki kurejesha sisi tunachotaka ni majina yao wale ambao wanafedha zetu, OCD hawa tunaondoka nao itakapofika wakati wa kufungua shule wote waanze shule", amesema DED Manoza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Anthony Philip, amesema kuwa wiki ijayo halmashauri yake itatoa shilingi milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari hiyo.