Jumatatu , 3rd Nov , 2014

Hamasa zimetolewa wakati wanafunzi wa kidato cha Nne nchini leo wakitarajia kuanza kuanza mitihani yao ya taifa, ambapo shauku ya wadau ni kuona kutakuwepo kwa ongezeko kiasi gani la kiwango cha ufaulu nchini hasa kwa Masomo ya Sayansi.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mh. Dk. Shukuru Kawambwa

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Nyirembe Munasa akizungumza na wazazi pamoja na waalimu wakati wa zoezi la kuchangia fedha za uanzishwaji wa maabara kwa baadhi ya shule za Sekondari, amesema tayari kasi ya ujenzi wa maabara imeonesha matumaini, kwani hadi hivi sasa jumla ya maabara 36 zipo katika shule mbalimbali za Arumeru.

Katika zoezi la kuchangia uanzishwaji na ukamilishwaji wa maabara katika shule za binafsi, tayari shule ya Sekondari The Voice iliyopo Arumeru, imefanikisha upatikanaji wa fedha pamoja na vifaa vyote vinavyohitajika kwaajili ya wanafuzi kujifunzia, ikiwa ni juhudi za wadau pamoja na serikali ya Wilaya kuhakikisha wanafunzi wanaochagua masomo ya sayansi wanafanya vizuri.

Mkurugenzi wa The Voice Daniel Mpanduzi, na wanafunzi wa shule hiyo, wamesema kiwango cha ufaulu wa masomo ya sayansi kimekuwa kikishuka, kutokana na ukosefu wa miundombinu na hivyo juhudi za Rais katika kuhamasisha Ujenzi wa Maabara, kutaibua hamasa mpya katika ufaulu wa masomo hayo.