"Mimi natishiwa sana, nitakimbilia wapi"- IGP

Alhamisi , 19th Nov , 2020

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, amesema kuwa mara baada ya kusikia aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA Tundu Lissu, kwamba anatishiwa na hatimaye kukimbilia ubalozini, alikiandikia barua chama chake kwamba afike polisi kwa ajili ya kueleza undani wa nani anayemtishia.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo hii leo Novemba 19, 2020, jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa usalama wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu na kwamba endapo mtu yeyote akitoa taarifa ya kutishiwa na akaomba ulinzi, yeye yuko tayari kumpa ulinzi wa familia yake.

"Hata alipokuja hapa nchini tumejitahidi sana kumpata tuweze kujua kitu gani kimefanyika lakini hakutaka, tumejitahidi sana mpaka kupeleka barua kwenye chama chake tunamuomba aje hata asindikizwe na Balozi, hivi ukitishiwa kwa maneno hata silaha jibu lake ni kukimbilia ubalozi, hata mimi nimeshatishiwa kwamba Kamanda Sirro leo tutakushughulikia sasa nakimbia kwenda ubalozi gani, inategemea na mipango mikakati yake",amesema IGP Sirro.

Aidha Kamanda Sirro amesema kuwa hawa watu wanaolalamika kuwa wanatishiwa huenda ukawa ni mpango mkakati wao wa kutafuta kuishi kwani kila mmoja anazo mbinu za kutafuta maisha.