Mgombea Urais, Demokrasia Makini kukomesha ubakaji

Jumapili , 18th Oct , 2020

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia Makini Mh. Cecilia Mmanga amesema endapo atapata ridhaa ya kuliongoza taifa la Tanzania atahakikisha watuhumiwa wa makosa ya ubakaji na ulawiti wanapewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia Makini Mh. Cecilia Mmanga.

Mh. Cecilia amesema hayo wakati akizungumza katika moja ya kampeni zake alizozifanya wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani ambapo amesema vitendo vya ulawiti na ubakaji kamwe hatovifumbia macho kwani vimekuwa vikisababisha kuharibu utu wa mtoto ikiwemo mmomonyoko wa maadili kwa taifa.

"Sitawafumbia macho wale wote wanaofanya vitendo vya ubakaji na ulawiti, wanakatisha ndoto za watoto wetu. Katika uongozi wangu sitowaacha salama", amesema Mmanga.

Kuhusu tozo wanazotozwa wananchi pindi wanapokwenda hospitali kuchukua maiti za wapendwa mgombea huyo amesema atahakikisha anaondoa gharama ambazo zimekuwa zikisababisha kero kubwa kwa Watanzania kote nchini.