Jumatano , 27th Apr , 2016

Miamala yenye thamani ya shilingi trilioni mbili kila mwezi, kupitia huduma ya kutuma na kupokea pesa ya M-Pesa inayotolewa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania Bw. Ian Ferrao

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo na mkuu wa mahusiano wa Vodacom Tanzania Bi. Rosalynn Mworia, wakati Kampuni ya mahesabu na ushauri wa masuala ya kifedha ya KPMG, ilipotoa ripoti ya mchango wa kiuchumi uliotokana na Vodacom Tanzania kati ya mwaka 2012 na 2015, ripoti inayoonyesha kuwa mchango wa kampuni hiyo katika uchumi ni mkubwa.

Kwa mujibu wa Bi. Mworia, ripoti ya KPMG inaonyesha kuwa Vodacom Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika maeneo mengi ikiwemo utoaji wa huduma za mawasiliano, huduma za jamii, fursa za ajira na kibiashara kwa idadi kubwa ya Watanzania pamoja na kuchangia takribani asilimia mbili ya pato la taifa kila mwaka.

"Tumekuwa tukifanya vizuri na hasa kuchangia kwenye uchumi kwa kutoa fursa nyingi za ajira pamoja na biashara hasa kwa Watanzania waliojiajiri kupitia biashara ya M-Pesa," alisema Bi. Mworia.

Awali katika maelezo yake, Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania Bw. Ian Ferrao amesema kampuni yake imekuwa ikitii na kulipa kodi kwa wakati na wala sio sehemu ya kampuni zinazokwepa kulipa kodi.

Kauli ya Bw. Ferrao imekuja kufuatia swali kutoka kwa wanahabari lililotaka kujua iwapo Vodacom ni sehemu ya kampuni zilizokwepa kodi kama ilivyoelezwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG.