Marehemu Eugene Mwaiposa enzi za uhai wake
Kwa mujibu wa Naibu Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai ambaye amelitangazia bunge leo majira ya saa 7 mchana, marehemu Mwaiposa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu.
Ndugai amesema kuwa kwa sasa msiba upo nyumbani kwake eneo la Chadulu Dodoma ambapo pia familia yake inasubiria hapo kwa ajili ya kuaga mwili wake shughuli ambayo itafanyika kesho (Jumatano).
Bunge limeahirishwa hadi keshokutwa saa 3 Asubuhi.
Marehemu Mwaiposa alizaliwa Novemba 23, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro mwaka 1960 na amefariki leo akiwa na umri wa miaka 54.
Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Nkweseto mwaka 1967 hadi 1974 na kujiunga na shule ya sekondari Masama mwaka 1976 hadi 1980 ambapo baadaye alipata elimu ya juu ya sekondari katika shule ya biashara ya Shinyanga (Shycom) mwaka 1981 hadi 1983.
Amefariki akiwa na shahada mbili za uzamili, moja ikiwa ni ya mahusiano ya kimataifa kiuchumi na (Masters in International Enomic Relations) na nyingine akiipata katika chuo kikuu cha Strathclyde, kilichoko Glasgow nchini Scotland.
Enzi za uhai wake amewahi kufanya kazi taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na benki ya CRDB, shule ya msingi Tumaini, Kipunguni SACCOS.
Amekitumikia Chama Cha Mapinduzi kwa nyazifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa mjumbe wa Umoja wa wanawake wa CCM UWT na mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM kupitia UWT kati ya mwaka 2008 na 2013.
Mungu ametoa Mungu ametwaa jina lake lihimidiwe. R.I.P