Alhamisi , 26th Mei , 2016

Mbunge wa Monduli Julius Laizer Kalanga (Chadema), amesema kuwa Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa hana hati miliki ya shamba lolote katika jimbo hilo bali ni upotoshaji wa taarifa alizopewa Waziri wa Ardhi,Wiliam Lukuvi na wasaidizi wake.

Mbunge wa Monduli Julius Laizer Kalanga (Chadema) akiwa na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.

Laizer ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma kufuatia habari zilizoandikwa kwenye vyombo vya habari kuwa serikali imemnyang’anya Edward Lowassa mashamba yake na kuwagawia wananchi jambo alilosema si kweli.

Amesema habari hizo zimemletea usumbufu mkubwa kutoka kwa wananchi wake kwani habari hizo siyo za kweli kwani ukweli uliopo ni kwamba shamba lililozungumzwa Bungeni ni shamba la Stein lililopo Makuyuni ambalo mmiliki wake alishafukuzwa nchini na serikali tangu mwaka 1980 na hati yake ilishafutwa lakini bado lilikuwa bado halijamilikishwa kwa wananchi.

Amesema shamba hilo la Stein lilishafutwa hati yake tangu mwaka 2005 lakini bado lilikuwa bado halijamilikishwa kwa wananchi na hiyo ndiyo iliyokuwa hoja ya msingi kwa serikali kuwa italimilikisha shamba hilo lini kwa wananchi.

Shamba la Manyara Ranchi lina ukubwa wa ekari 44,930 sawa na hekta 17,000 ambalo lilikabidhiwa kwa wananchi tangu mwaka 2000 kwa ajili ya malisho ya wanyama wakati wa kiangazi na njia ya wanyamapori shamba hilo lipo katika vijiji viwili vya Oltukay na Esilalei katika jimbo la Monduli ambapo shamba la stein Seed Valley lipo Makuyuni.