Jumanne , 14th Feb , 2017

Mbunge wa Singida Magharibi Elibariki Kingu akiwa ameambatana na mke wake Bi. Anna Jacob hii leo wametema madini kama fundisho kwa wanandoa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya 'Siku ya Wapendanao' (Valentine's Day), tarehe 14 Februari kila mwaka.

Mbunge wa Singida Magharibi Elibariki Kingu na Mkewe Bi. Anna Jacob

Wawili hao wamefunguka mengi kuhusu mahusiano yao, walipoambatana pamoja katika kipindi East Africa Breakfast cha EA Radio kinachoruka saa 11:00 alfajiri hadi saa 3:00 Asubuhi.

Huku wakionesha jinsi wanavyopendana, wawili hao wamesimulia jinsi walivyokutana, ambapo wamesema kuwa walikutana kwenye msiba, na kila mmoja akatokea kumpenda mwenzake bila kujali hali zao za kimaisha, takriba miaka 9 iliyopita.

Anna ametoa ujumbe kwa mabinti ambao hawajaolewa kwa kumesema katika mapenzi, haitakiwi mwanamke kumpenda mwanaume kwa sababu ya mali na ndiyo maana yeye alimpenda Kingu wakati huo hajawa mbunge, huku akibainisha kuwa alilazimika kubadili dini, ili wawe pamoja.

Pia Bi. Anna ambaye kitaaluma ni mtaalam wa masuala ya benki (Banker) amesisitiza suala la uaminifu katika ndoa, akiwataka watu wote walio katika ndoa watambue kuwa kilichowaunganisha ni uaminifu, hivyo hawapaswi kuvunja kiapo hicho huku akiweka wazi kuwa kosa pekee ambalo hawezi kulisamehe kwa mume wake ni la kuvunja uaminifu.

Akizungumzia ratiba za mume wake kama Mbunge, amesema kuwa hazimkwazi na tayari anazifahamu, na kwamba hata wakati anafikia kugombea ubunge alimshirikisha, na yeye alimpa sapoti ya kutosha.

Kwa upande wake Kingu, ameshauri wanandoa kuwa na uwazi katika kila jambo ikiwa ni pamoja na mali pamoja na kipato cha kila mmoja, huku akitupia lawama wanaume wengi ambao huwa na tabia ya kuwaficha wake zao baadhi ya mambo kuwa ni hatari na ni sababu ya ndoa nyingi kuvunjika, pamoja na wanaume wengi kufariki kwa shinikizo la daumu na kuacha wanawake wengi wakiwa wajane

Pia Kingu amewasihi wanandoa kuwa na moyo wa kuvumiliana na kuchukuliana mapungufu ili kulinda ndoa, ambapo ametolea mfano jinsi mke wake alivyombadilisha kutoka kuwa na tabia ya hasira za haraka hadi hakuwa mtulivu, na sasa anajigamba kuwa ni baba bora kutokana na aina ya mke aliyempata.

Sikiliza hapa Mazungumzo yalivyokuwa ndani ya Studio za EA Radio, katika kipindi cha EA Breakfast kinachoongozwa na Irene Tillya, Shaaban Lupa na Songa wa Songa.................................