Jumanne , 15th Sep , 2020

Tanzania imeruhusu nchi 15 kupitia balozi zao kuleta waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 28 mwaka huu, baada ya balozi hizo kuwasilisha maombi na kufuata taratibu zilizowekwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi.

Hayo yamesemwa  leo Septemba 15,2020 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Profesa Palamagamba Kabudi  jijini Dar es Salaam, wakati akifanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya Balozi Manfred Fanti, ambapo amesema kuwa kwa mara ya kwanza uchaguzi huo unafanyika kwa kutumia fedha za ndani na sio wahisani kama miaka iliyopita.

Mbali na Balozi wa Ulaya Profesa Kabudi pia amekutana na Balozi wa Italia Roberto Mengoni, na Balozi wa Poland ambapo amekabidhi vitabu vya sheria ,kanuni na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi ili kuwapa fursa ya kufahamu jinsi uchaguzi unavyoendeshwa. 

Kwa upande wake  Balozi wa Umoja wa Ulaya Manfred Fanti amesema, ameridhishwa na namna kampeni zinazofanyika kwa uhuru na amani na sasa wanajiandaa na uangalizi wa uchaguzi huo.

Naye Balozi wa Italia hapa nchini Roberto Mengoni amesema, anavutiwa na namna ambavyo vyombo vya habari vimekuwa vikitoa nafasi kwa wagombea wote bila ubaguzi na ambavyo Watanzania wanajitokeza kusikiliza sera na kudai kuwa ana imani kiongozi atakayechaguliwa atatokana na utashi wa wananchi.