Masauni atoa tamko vurugu zinazoendelea Zanzibar

Jumapili , 18th Oct , 2020

Naibu Waziri wa Mambo ya  Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, ametoa onyo kwa watu wenye nia ovu ya kuvuruga mwenendo wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28,mwaka huu.

Naibu Waziri wa Mambo ya  Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.

Naibu waziri Masauni amezungumza hayo  hii leo baada ya kuwatembelea majeruhi  saba waliopo katika hospitali ya Micheweni, waliojeruhiwa baada ya kuzuka kwa vurugu katika eneo la Kwale, Wilaya ya Micheweni, Pemba, zilizohusishwa na itikadi za kisiasa ambapo amekemea vikali matukio hayo.

''Niwasihi sana wananchi kuepuka kuchochewa kuvunja sheria za nchi kuelekea katika uchaguzi mkuu sababu serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba atakayekiuka sheria za nchi basi sheria itafuata mkondo wake''amesema Masauni

Kwa upande wa Kamishna Mkuu wa Jeshi la  Polisi Zanzibar, CP Mohammed Haji Hassan, amesema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi  ambapo watu 58 wanashikiliwa kutokana na tukio hilo.