Jumanne , 5th Jan , 2016

Waziri wa Maliasili na Utalii Pro. Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa mipango na matumizi ya rasilimali wa wakala wa misitu nchini Mohamed Kilongo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Pro. Jumanne Maghembe.

Waziri Maghembe amechukua hatua hiyo leo baada ya kugundua uzembe katika usimamizi wa rasilimali za wakala hao wa misitu ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi huyo kushindwa kuwasimamia maafisa maduhuli ambao wameshindwa kukusanya na kuwasilisha maduhuli ya serikali kwa wakati.

Aidha Prof. Maghembe ameagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), kupitia upya vitabu vyote vya mapato ya wakala huo wa misitu nchini kwani takwimu zinaonesha kuwa kuna maafisa maduhuli hawajawasilisha fedha za serikali toka mwaka 2004.

Wakati huo huo waziri Maghembe amewataka maafisa wa wakala wa misitu waliopanga ofisi nje ya jengo la wakala wa misitu la Mpingo House warudi haraka katika jengo hilo ndani ya siku 7 zijazo pamoja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuipa hasara serikali.