Jumatatu , 16th Jan , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameeleza sababu ya kupanda kwa bei ya vyakula masokoni, na kusema hali hiyo inasababishwa na uhaba wa chakula katika nchi jirani

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa safari ya Dar - Dodoma ya ndege za ATCL iliyofanyika mjini Dodoma leo, na kutolea ufafanuzi suala la njaa

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo mjini Dodoma na amekiri baadhi ya mazao katika masoko yamepanda bei kutokana na uhitaji wa nchi za jirani zikiwamo za Afrika Mashariki kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Kenya, Somalia na Sudan ambazo zinategemea kupata chakula kutoka Tanzania.

Pia amesisitiza kuwa nchi haijakumbwa na baa la njaa huku amewataka Watanzania utosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la  kupandisha bei za vyakula.

“Mwaka jana nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni tatu hali iliyopelekea baadhi ya Wabunge na wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi, ambapo Serikali ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha ya chakula,” amesema.

Amesema baada ya kutolewa kwa kibali hicho tani milioni 1.5 ziliuzwa nje ya nchi na kiasi cha tani milioni 1.5 zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba ambapo tayari wameruhusu ziuzwe hapa nchini ili kupunguza kupanda kwa bei za vyakula nchini. 

“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” amesema.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo amewaomba wananchi kuzitumia kwa kulima mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame.

 

 

Sauti ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa