Jumanne , 23rd Mei , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya  Kilimo Tanzania (TADB) kuwekeza zaidi katika kukopesha wakulima waweze kununua matrekta yatakayowasaidia kulima kilimo cha kisasa na kuinuka kiuchumi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kiwanda cha kuunganisha matrekta URSUS-TAMCO, Kibaha mkoani Pwani.

Majaliwa amesema hayo leo alipokuwa akitembelea eneo la viwanda la TAMCO lililoko katika kitovu cha mji katika halmashauri ya mji wa Kibaha na kujionea hatua za awali za uunganishaji matrekta na zana zake unaofanywa kwa kushirikiana na wataalamu kutoka kampuni ya URSUS ya Poland.

Amesema ameridhishwa na uwepo wa viwanda katika mkoa wa Pwani na kuwa ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo hususani wakulima hivyo endapo watakopeshwa matrekta wataweza kuongeza tija katika kilimo na kuinuka kiuchumi hatimaye  kuleta matokeo  chanya.

Mkurugenzi Mwendeshaji  wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi Mkucha amesema hadi sasa tayari yameunganishwa matrekta yapatayo 92 na kuwa kwa awamu ya kwanza ya mradi huo unatarajia kuunganisha jumla ya matrekta 2400.

Amesema mradi huo umegharimu kiasi cha dola milioni 55 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda na kufunga mitambo na vifaa vya kuunganisha matrekta.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema nchi ina viwanda vikubwa vipatavyo 393 na kati ya hivyo 84 viko mkoani Pwani, hivyo alizitaka halmashauri kuepuka kutoza tozo kubwa la viwanja ili kuwavutia wawekezaji, waweze kumudu gharama na kuendelea kuwekeza zaidi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.