Magufuli amkumbuka Makonda kwa hili

Jumanne , 13th Oct , 2020

Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli, amesema kuwa mtu wa kwanza aliyeomba ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Ubungo ni aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, na ndipo ujenzi huo ulipoanza.

Kushoto ni aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kulia ni mgombea urais kupitia CCM Dkt John Magufuli.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 13, 2020, wakati akiomba kura kwa wakazi wa Ubungo na Kibamba, ambapo amewataka wasifanye makosa ya kumchanganyia na badala yake wachague madiwani na wabunge kutoka CCM.

"Hospitali ya wilaya ya Ubungo mnakumbuka siku ile tupo kwenye sherehe Airport, iliombwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, mpaka RC anaomba mbunge alikuwa wapi kuomba, tukaijenga kwa sababu Ubungo na Kibamba ilikuwa kama watoto yatima, msiendelee kuwa yatima", amesema Dkt Magufuli.

Katika hatua nyingine Dkt Magufuli amesema kuwa endapo Ubungo na Kibamba watamchagulia madiwani na wabunge kutoka CCM, atahakikisha anajenga makao makuu ya wilaya ya Ubungo kama ilivyo Kigamboni.

"Tupeni kura, msinikatishe tamaa ndugu zangu aombaye hupewa tumebembeleza mno basi mtupe, na anayepewa lazima ameoma ndiyo maana tumekuja hapa kwa unyenyekevu, mniletee madiwani wa CCM mniletee vijana hawa wawili Profesa Mkumbo na Mtemvu, mkiniletea hawa hamtajuta", ameongeza.