Jumamosi , 27th Feb , 2021

Maabara ya Taifa imeondolewa katika orodha ya chaguo (option) la vituo vya kutolea sampuli za kupima COVID -19 kwa njia ya RT - PCR kwa wasafiri katika mfumo wa kutuma miadi wa pimacovid.moh.go.tz. 

Mfano wa sampuli iliyochukuliwa kwaajili ya kufanyiwa vipimo vya Covid-19.

Kwa mabadiliko hayo, kuanzia Machi Mosi, 2021, wasafiri wote wanaohitaji kipimo hiki wanaelekezwa kupata huduma ya kuchukulia sampuli katika Vituo / hospitali za Mjini Dar es Salaam na Mikoani kote (ona kiambatanisho) na baadae kutumiwa vyeti kwa njia ya mfumo wa TEHAMA. 

Maelekezo hayo yametolewa leo na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, tangazo lililosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Afya), Gerard Chami ambaye  amesisitiza haitaruhusiwa tena wasafiri kwenda moja kwa moja Maabara Kuu iliyoko Mabibo Dar es Salaam, kwa ajili ya kipimo au majibu au vyeti.

 "Lengo ni kuongeza ufanisi wa majibu na kuondoa mrundikano wa wasafiri katika maabara kuu," amebainisha, Maabara ya Taifa imekuwa ikichukua sampuli, ikizichakata, kuzipima, kutoa majibu pamoja na kuandaa vyeti kwa wasafiri  katika kutekeleza jukumu hilo, kumekua na wasafiri wengi wanaofika kwenye Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na kusababisha msongamano mkubwa katika eneo la maabara”, imesema taarifa ya Wizara

 Kwa mabadiliko mapya, Chami amesema wasafiri wanakumbushwa tena kuchukuliwa sampuli siku tatu (masaa 72) kabla ya kusafiri ili kuepuka kuchelewa kwa vyeti. 

"Wasafiri wote watatakiwa kwenda kwenye vituo vya kuchukulia sampuli kama ilivyotolewa kwenye Mwongozo wa Ushauri kwa Wasafiri (Travellers Advisory). Hivyo kuanzia tarehe 01 Machi, 2021 Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii haitapokea wasafiri na kuwachukua sampuli na badala yake itabaki na jukumu la kupiman kutoa vyeti ikiwa ndio jukumu lake la msingi," amesisitiza Chami.